Ayatullah Alireza Arafi, Mkuu wa Hawza za Elimu nchini Iran, alitoa wito huo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari wa Shirika la Habari la Hawza, pembezoni mwa ziara yake katika Makumbusho na Kituo cha Nyaraka za Hawza na Taasisi ya Maulamaa.
Akifafanua kuhusu ombi hilo la jumla, alisisitiza: "Kwa kupitia Shirika la Habari la Hawza, ninatoa wito kwa Maraji' wakuu, wanazuoni mashuhuri na watu mbalimbali ambao wanamiliki nyaraka zinazohusiana na Hawza na taasisi ya Maulamaa, au zinazohusu mji wa Qum, mabadiliko na maendeleo mbalimbali yaliyotokea katika Harakati ya Imam na Mapinduzi ya Kiislamu, wazikabidhi nyaraka hizo katika Makumbusho na Kituo cha Nyaraka za Hawza, iwe ni nyaraka halisi au nakala zake. Hii ndiyo rai na ombi letu la jumla."
Mkuu wa Hawza alisisitiza kuwa; Shirika la Habari la Hawza linapaswa lenyewe kushughulikia suala hili kwa kufanya kazi ya uhamasishaji na uelimishaji, ili kupitia wito huo, wananchi, watu mashuhuri na wanazuoni wahimizwe kushiriki katika kuimarisha na kuongezea nyaraka katika kituo hicho.
Hazina kubwa yenye nyaraka milioni mbili za kihistoria zisizo na kifani
Mjumbe wa Baraza la Wanazuoni wa Baraza la Kulinda Katiba ya Iran, alizungumzia ukubwa wa nyaraka zilizokusanywa na kusema: "Namshukuru Mwenyezi Mungu, kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na ndugu zetu, hivi sasa wanasema kuwa wamefanikiwa kukusanya takribani nyaraka milioni mbili. Nyaraka hizi milioni mbili zina ukubwa na umuhimu ambao thamani yake haiwezi kabisa kukadiriwa wala kupangiwa bei. Tunatumai kuwa kazi hii na mwelekeo huu vitaendelea bila kusimama."
Makumbusho ya nyaraka: Kioo halisi kinachoakisi utambulisho wa wanafunzi wa Hawza
Ayatullah Arafi, akifafanua vipengele mbalimbali na majukumu ya Kituo cha Nyaraka za Hawza na Taasisi ya Maulamaa, alisema: "Hiki ni kituo jumuishi ambacho kina uwezo wa kuendeleza na kuinua utamaduni wa Hawza pamoja na utamaduni wa nchi kwa ujumla. Aidha, kinahesabika kuwa hazina kubwa sana kwa ajili ya kufanya tafiti, uchunguzi wa kitaaluma na usomaji wa kielimu."
Mkuu huyo wa Hawza nchini Iran aliendelea kusema: "Jukumu kuu la kituo hiki ni kujenga upya utambulisho wa wanafunzi wa Hawza. Kwa hakika, makumbusho haya yanajenga utambulisho wa wanafunzi wa Hawza. Makumbusho yanayojenga utambulisho ni yale ambayo mwanafunzi wa Hawza anapokuja, anaweza kuiona historia ya wakati uliopita ikiwa katika sura halisi mbele yake, na kisha kuijenga upya historia hiyo na kuifanya kuwa sehemu ya utambulisho wake binafsi."
Taa angavu ya kuifafanua na kuitambulisha historia ya Hawza na taasisi ya Maulamaa
Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza, akiwapongeza na kuwashukuru wasimamizi wa mradi huo, alisema: "Ni kwa mtazamo huu ndipo tulipowahamasisha ndugu zetu, nao wakaonesha juhudi kubwa na azma ya hali ya juu. Tunatumai, Mwenyezi Mungu akipenda, kituo hiki kitakuwa taa angavu ya kujenga utambulisho, kuimarisha utamaduni na kuinua kiwango cha uelewa wa jamii kuhusu historia ya taasisi ya Hawza na taasisi ya Maulamaa."
Ayatullah Arafi aliongeza: "Tunatumai kuwa kwa wanazuoni, wasomi mahiri na wananchi kwa ujumla kuitikia wito huu, tutashuhudia hazina hii ya kitaifa ikiendelea kuimarika na kuwa na utajiri mkubwa zaidi.
Kulinda na kuhifadhi urithi wa maandishi na simulizi za Hawza inahesabika kuwa hatua imara katika juhudi za kuhifadhi na kudumisha utamaduni halisi wa Kiislamu na Mapinduzi ya nchi. Hatua hii ya kudumu na yenye thamani kubwa itachangia kuchora kwa usahihi na uwazi zaidi taswira ya mustakabali wa Hawza kwa kuzingatia ushahidi na vielelezo sahihi vya kihistoria."
Maoni yako